lnawezekana likawa tukio baya lililoacha gumzo na simanzi baada ya
mfanyabiashara wa mjini Moshi, Romani Shirima (74), kujiua kwa kujilipua
kwa petroli nje ya nyumba yake.
Habari kutoka kwa mashuhuda wa tukio hilo zinasema mfanyabiashara huyo
alijifunika kwa blanketi, kisha kujimwagia petroli na kutumia kibiriti
kuwasha moto ambao ulimlipua na kusababisha kifo chake.
Ingawa hakuna taarifa rasmi ya nini kiini cha mfanyabiashara huyo
kuchukua uamuzi huo mgumu ulioacha maswali mengi, lakini baadhi walidai
ni msongo wa mawazo uliotokana na madeni.
Hili ni tukio la pili kwa mfanyabiashara mkazi wa mkoa wa Kilimanjaro,
kwani miaka kadhaa iliyopita, mfanyabiashara anayemiliki hoteli eneo la
Marangu alijilipua kwa petroli akiwa katika gari lake.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Wilbroad Mutafungwa alisema jana
kuwa tukio hilo lilitokea juzi, saa 11.25 asubuhi maeneo ya Mjohotoni.
Alisema, mfanyabiashara huyo ni mmiliki wa shule ya sekondari ya Merinyo
iliyopo mjini Moshi, na kusema kuwa aliamka asubuhi nyumbani kwake na
kujimwagia mafuta hayo na kisha kujilipua na kiberiti.
Kamanda Mutafungwa alisema chanzo cha kifo chake bado hakijafahamika
ingawa kuna maneno yanayoongelewa na watu, lakini hawawezi kuyachukua
moja kwa moja na kwamba jeshi hilo linachunguza ili kubaini chanzo
chake.
Taarifa za tukio hilo la aina yake zimekuwa gumzo katika maeneo
mbalimbali ya mji wa Moshi na vitongoji vyake, hasa njia aliyoitumia
kukatisha uhai wake.
No comments:
Post a Comment