Waziri wa Afya Ummy Mwalimu atoa msamaha wa matibabu na vipimo kwa
watoto ambao wamefanyiwa vitendo vya ulawiti na kubakwa. Pia amezitaka
hospitali za serikali pindi watoto hao wapelekwapo hospitali wapewe
kipaumbele kwenye kupata vipimo na tiba.
Msamaha huo umekuja baada ya vitendo vya ulawiti na ubakaji kushamiri
kwa kasi ambapo imeripotiwa kuwa matukio ya ubakaji na ulawiti
yanayoripotiwa vituo vya polisi yamefikia 15 kwa siku.
Wazazi wengine wamekuwa wakikosa matibabu ya watoto wao kutokana na
gharama kubwa za vipimo na dawa ambavyo vimekuwa vikifikia na kuzidi
250,000 kwa baadhi ya hospitali hivyo wazazi wa kawaida kushindwa kumudu
na kuacha liende tu.
Pia waziri wa afya amesema kuwa atakutana na waziri wa sheria na katiba
na mwanasheria mkuu ili waone namna ambavyo wanaweza kufanya mchakato wa
kuweka makosa ya ubakaji na ulawiti wa watoto kuwa kwenye makosa yasiyo
na dhamana.
Waziri Ummy Mwalimu amesema atawaandikia barua waganga wakuu wa mikoa na
wilaya kuhusu matibabu hayo. Pia ameahidi kutoa namba maalum ambayo
watu watakuwa wanaripoti endapo watakuwa wametozwa gharama yoyote.
Waziri pia amepiga mkwara kwa wazazi wanaomaliza kesi hizi nje ya
mahakama kwa kupewa hela yoyote, amesisitiza kuwa hela haiwezi kuwa na
thamani kuliko utu wa watoto wetu.
Maoni yangu:
Ni hatua nzuri sana hasa ukizingatia kuwa vitendo hivi vimeshamiri na
wazazi wengi wamekuwa wakiogopa kuwapeleka watoto hospitali kutokana na
mlolongo kuanzia polisi na mpaka hospitali.Hatua hii itapelekea vitendo
hivi kuripotiwa kuliko awali.
Kuhusu makosa ya ulawiti na ubakaji kuwa kwenye makosa yasiyo na dhamana
nayo ni habari njema maana tumeshuhudia jinsi wabakaji hao wajitapavyo
pindi wapatapo dhamana, juzi juzi kuna mbakaji kapata dhamana na kuamua
kushona suti sare na mkewe na kusherekea.
No comments:
Post a Comment