Watumishi 34 wa mahakama wakiwemo mahakimu 11, wamefukuzwa kazi kutokana na makosa mbalimbali ya kinidhamu.
Aidha, Tume ya Utumishi wa Mahakama inaendelea kujadili hatma ya
mahakimu 30, waliokuwa wanatuhumiwa kuhusika na rushwa na kushinda zao
mahakamani ili kuangalia kama walifanya makosa ya kinidhamu.
Jaji Mkuu, Mohammed Chande Othman alisema hayo Dar es Salaam jana wakati
akizungumza na waandishi wa habari baada ya kupokea taarifa za ukaguzi
wa mahakama pamoja na uendeshwaji wa mashauri.
Othman alisema watumishi hao, wamefukuzwa kutokana na uamuzi wa kikao
cha Tume ya Mahakama, kilichofanyika Agosti 18, mwaka huu baada ya
kushughulikia masuala mbalimbali ya kinidhamu.
“Tumewafukuza mahakimu wakazi wafawidhi, mahakimu wa mahakama za
Mwanzo za Rombo, Temeke, Bahi na Chamwino na watumishi wengine 23. Hii
ni idadi ndogo ambayo ni sawa na asilimia 0.005 ya wafanyakazi wote
lakini kwa mahakama ni doa kubwa,” alisema Jaji Mkuu.
Alisema mahakimu hao wamefukuzwa kwa makosa mbalimbali ya kinidhamu,
ikiwemo kutumia muhuri wa mahakama kinyume cha taratibu, kuathiri
utendaji wa haki kwa kumsaidia mtu kufungua kesi moja katika mahakama
mbili pamoja na kufungua kesi ya mirathi bila kuwa na hati ya kifo.
Aliongeza kuwa kuna makosa ya kisheria ambayo jaji au hakimu akikosea
kutumia kifungu cha sheria hawajibishwi, lakini kuna makosa ya kinidhamu
ambayo yanaondoa sifa ya kuwa hakimu au jaji.
Kuhusu mahakimu walioshinda kesi za rushwa mahakamani, Jaji Chande
alisema mahakama inaweza isiwakute na hatia, lakini Tume itaangalia kama
walifanya vitendo vya ukosefu wa nidhamu na kuwawajibisha.
Aidha, alisema mahakimu wengine 32 waliokuwa wanakabiliwa na kesi za
jinai na kushinda kesi mahakamani, wanafunguliwa mashitaka ya kinidhamu
katika Kamati ya Maadili ya Maofisa wa Mahakama kwa sababu inawezekana
hawajapatikana na hatia ya kosa la jinai, lakini kama kuna vitendo vya
ukosefu wa maadili watawawajibisha kimaadili.
Mahakama Maalumu ya Ufisadi
Katika hatua nyingine, Mahakama Maalumu ya Ufisadi na Uhujumu Uchumi
imeanza rasmi na wiki ijayo Kanuni za Uendeshaji wa mahakama hiyo,
zinatarajiwa kuchapishwa.
Jaji Mkuu Othman alisema mahakama hiyo, imeanza rasmi Julai 18 mwaka huu
baada ya Rais John Magufuli kusaini sheria ya uanzishwaji wa mahakama
hiyo.
“Wiki ijayo tutachapisha kanuni mbalimbali za uendeshwaji wa mahakama
hiyo, ikiwemo jinsi ya kulinda mashahidi pamoja na taratibu za ufunguaji
wa kesi,” alisema Othman.
Alisema mahakama hiyo itakuwa na majaji wa kutosha ili kufanya kazi kwa
uadilifu na kumaliza kesi kwa wakati, pia haitakuwa ikiahirisha kesi
mara kwa mara.
Kuhusu utendaji kazi wa mahakama, Jaji Mkuu alisema mahakama haiwezi
kutoa haki kama itakuwa inajificha au kuendeshwa kwa siri, ndiyo maana
kwenye maboresho ya mahakama, wameamua kuwapa fursa wananchi kutoa
mapendekezo au kero zao kupitia namba za simu pamoja na barua pepe.
Kesi za uchaguzi
Awali akiwasilisha taarifa za utendaji wa Mahakama Kuu, Mahakama za
Hakimu Mkazi, Wilaya na za Mwanzo, Msajili wa Mahakama Kuu, Ilvin Mugeta
alisema baada ya uchaguzi, walipokea kesi 247 za uchaguzi, 53 za
kupinga matokeo ya ubunge na 194 za udiwani.
Mugeta alisema tayari wameshamaliza kesi 234, zimebaki 13, lakini hadi
kufikia Desemba mwaka huu kesi zote zitakuwa zimemalizika.
Aidha, alisema tathmini waliyoifanya inaonesha kesi zilizopo zinawiana
na mahakimu, na kama watawezeshwa kwa vifaa vya kutendea kazi hadi
Desemba mwaka huu watamaliza kesi zote zilizofunguliwa mwaka huu.
Mahakama ya Rufaa
Kwa upande wake, Msajili wa Mahakama ya Rufaa, John Kahyoza alisema
kiwango cha kumaliza mashauri katika Mahakama ya Rufaa kimeongezeka, pia
wana lengo la kuhakikisha nakala za hukumu zinapatikana siku hukumu na
ndani ya siku tatu zitapatikana kwenye tovuti ya Mahakama ya Tanzania.
Aidha, aliwaomba wananchi watoe ushirikiano ili rufaa zisikilizwe na
kuisha mapema, kwa sababu kuna watu wanashindwa kufika mahakamani bila
sababu za msingi au kutoa visingizio jambo linalosababisha rufaa zao
kuchelewa.
Umuhimu wa mahakama
Katika hotuba yake kwenye Maadhimisho ya Siku ya Sheria Februari 4,
mwaka huu, Rais Magufuli alisema anaitegemea sana Mahakama na aliwaambia
majaji na mahakimu nchini kuwa:
“Nawaomba waheshimiwa majaji na waheshimiwa mahakimu, muitangulize
Tanzania kwanza. Mkiitanguliza Tanzania kwanza tutaweza kufika mbali na
tutaweza kuwasaidia watanzania wengi.
"Nimeamua nchi iende, na itaenda. Anayefikiri ataikwamisha, atakwama
yeye kwa sababu Mungu yuko pamoja na mimi. Na watu ninaowategemea sana
ni Mahakama. Mahakama unafunga kila mmoja. Hata Rais nikitaka kufungwa
na Mahakama, nafungwa. Mbunge anafungwa, nani anafungwa, nyinyi ndio
wenyewe”.
No comments:
Post a Comment