Mamlaka
ya Mapato Tanzania(TRA) imekamata akaunti za Kampuni ya Sahara Media
Group ambayo inamiliki vituo vya habari vya Star TV, Kiss FM pamona
Radio Free Africa kwa kushindwa kulipa deni la Sh4 bilioni kama kodi
iliyopaswa kulipwa na kampuni hiyo.
Taarifa zilizosambaa kupitia mitandao ya kijamii zimeeleza kuwa akaunti
zote za kampuni hiyo zimefungiwa mpaka pale watakapolipa deni hilo,
lakini kampuni hiyo imetoa ufafanuzi.
Ujumbe huo uliongeza kuwa kampuni hiyo imefikishwa mahakamani na benki
moja hapa nchini kwa madai ya kutaka kulipwa Sh600 milioni, baada ya
kuingia makubaliano ya kulipa wafanyakazi wake mishahara pamoja na
mikopo lakini mpaka sasa imeshindwa kurejesha fedha hizo.
Hata hivyo, akizungumzia suala hilo mwenyekiti mtendaji wa kampuni ya
Sahara, Anthony Diallo alikiri mamlaka hiyo kufungia akaunti ya kampuni
yake.
Diallo ambaye ndiye mmiliki wa kampuni hiyo alisema ni akaunti moja tu
iliyofungiwa na kwamba anaamini baada ya kukutana na kufanya mazungumzo
na mamlaka hiyo watafikia muafaka ili biashara ziendelee kama kawaida.
“Tutalimaliza hakuna kitakachoenda mrama,” alisisitiza Diallo ambaye
aliwahi kushika nyadhifa mbalimbali serikalini ikiwamo nafasi ya Waziri
wa Maliasili na Utalii na Naibu Waziri wa Maji, Maendeleo ya Mifugo
katika Awamu ya Nne chini ya Rais mstaafu Jakaya Kikwete.
Amesema deni la TRA linatokana na kodi iliyopatikana baada ya ukaguzi wa
vitabu kwa miaka mitatu. “Ni ukaguzi wa kawaida hufanyika kama
taratibu. Sasa kwa sababu ya kuhamisha matangazo yetu kutoka analojia
kwenda digitali ilibidi tukope benki, ujenzi na kumaliza mradi imechukua
miaka mitatu. Wakati wote tumekuwa tukilipa riba benki na zinazobaki
toka mauzo ya matangazo tunalipa mishahara, umeme na malipo ya kodi za
kawaida,”alisema.
“Ni kawaida ila wamefanya hatua za kutuaibisha tu. Kampuni yetu ya
ving’amuzi ni ya Kitanzania na mapato yote yanaingia nchini wakati
kampuni nyingine kubwa zote ni za kigeni kutoka China, Afrika Kusini,
Mauritius na Kenya! Ukweli sisi tunahitaji kusaidia nchi kiuchumi na
kutuharibia ni hasara kwa nchi.”
Hata hivyo, baadaye jioni mwenyekiti huyo aliliambia Mwananchi kuwa
tayari wamefanya mazungumzo na mamlaka hiyo na kukubaliana jinsi gani
watalipa deni hilo.
“Tumezungumza nao wametuelewa na kutupa namna ya kulipia, sisi ni
wafanyabiashara ni lazima tufuate taratibu za biashara ili biashara yetu
iende vizuri,”.
Alipoulizwa kuhusu taarifa hizo, Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa
Mlipakodi, Richard Kayombo aliomba apewe muda aulize kutokana na yeye
kuwapo safarini.
“Taarifa hizo sina kwa sababu nipo safarini Ngorongoro naomba niulizie ofisini nitakurudia nikupe jibu,” alisisitiza Kayombo.
No comments:
Post a Comment