Chama
cha ACT-Wazalendo kimetoa taarifa yake kuhusu mwenendo wa serikali ya
awamu ya tano mara baada ya kumalizika kwa kikao cha kamati kuu
kilichoketi Jumatatu ya Septemba, 5, ambapo kimezungumzia hali ya
kisiasa, hali ya kiuchumi na kuzungumzia umoja wa kitaifa.
Akielezea kuhusu hali ya kiuchumi Kiongozi Mkuu wa ACT, Zitto Kabwe
amesema kwa kipindi ambacho Rais Magufuli amekuwa madarakani kasi ya
ukuaji wa uchumi ambayo ilikuwepo awali imepungua kwa asilimia nne
kutoka asilimia tisa hadi asilimia tano jambo ambalo halijawahi kutokea
kwa kipindi kirefu katika historia ya Tanzania.
“Kamati Kuu imeshtushwa na hali ya kuanza kudorora kwa shughuli za
uchumi katika kipindi cha miezi 10 ya utawala wa awamu ya tano, kwa
mfano; kwa robo ya mwaka 2015 yaani Oktoba hadi Disemba taarifa zilizopo
katika tovuti ya Benki Kuu ya Tanzania zinaonyesha pato la taifa
lilikuwa likipanda kwa asilimia tisa,
“Katika robo ya kwanza ya mwaka 2016 yaani Januari hadi Machi kasi ya
ukuaji wa pato la taifa ilishuka hadi asilimia 5.5, hii inamaanisha kuwa
ukuaji wa shughuli za kiuchumi katika kipindi cha miezi 6 ya mwanzo ya
utawala wa awamu ya tano chini ya Rais Magufuli imepungua kwa asilimia
4,” alisema Zitto.
Zitto alisema kuwa kutokana na kupungua kasi ya ukuaji wa uchumi Kamati
Kuu ya ACT imetoa mapendekezo kwa serikali ambayo inaamini kama
yakifanyiwa kazi basi itaweza kuimarisha hali ya uchumi na kuwa na kasi
kama ilivyokuwa awali.
“Tunaitaka serikali izingatie sayansi ya uchumi katika kuendesha uchumi
wa nchi. Uamuzi wa CCM wa kuitelekeza serikali yake kwa mwanasiasa mmoja
anayedhani ndiye anayejua kila kitu na yeye kugeuka kuwa mshauri wa
washauri wa uchumi itasambaratisha uwekezaji nchini na kuua kabisa
juhudi za miaka 20 ya kuvutia wawekezaji na kujenga uchumi,” alisema
Zitto.
No comments:
Post a Comment