Jeshi
la Polisi Mkoa wa Mara linamshikilia Julita Lucas (30), mkazi wa kijiji
cha Masinki Wilaya ya Serengeti kwa tuhuma za kufanya biashara haramu
ya kusafirisha binadamu anaowauza kuanzia Sh150,000 hadi Sh300,000.
Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Ramadhani Ng’anzi amesema Septemba 3, saa
9.00 alasiri, Lucas alikutwa akiwa na wasichana watano (majina
yamehifadhiwa) aliokuwa amewaficha nyumbani kwake kwa lengo la kuwauza
na wengine kuwaozesha kwa wanaume wenye kuhitaji.
Amesema baada ya mama huyo kuhojiwa alikiri kufanya biashara ya kuuza
wasichana kwa bei ya kati ya Sh 150,000 hadi 300,000, kwa kuangalia
ukubwa wa umbo na siyo umri.
“Baada ya kufanya mahojiano na wasichana hao wenye umri kati ya miaka 15
hadi 28, walisema wametokea katika kijiji cha Muhejangila Wilaya ya
Karagwe Mkoa wa Kagera,” amesema.
Kamanda Ng’anzi amesema polisi wanaendelea na uchunguzi dhidi ya mama
huyo, ili kubaini mtandao wa biashara hiyo haramu ya binadamu.
“Tunaendelea kumuhoji, tunataka kujua iwapo kituo cha mwisho cha
biashara hiyo ni hapa ndani tu au ni hadi nje ya nchi , biashara hiyo
ilianza lini na idadi ya wasichana waliokwisha uzwa na waliuzwa wapi,”
Kamanda Ng’anzi alisema baada ya upelelezi kukamilika, mama huyo atafikishwa mahakamani kujibu tuhuma hizo.
No comments:
Post a Comment