RAIA wa China aliyetambulika kwa jina Zhu Yush (27), amekufa wakati akipanda Mlima Kilimanjaro.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kilimanjaro, Willbrod
Mutafungwa, Yush aliyekuwa akitalii nchini, alikufa Septemba 7, mwaka
huu saa 7:00 mchana, katika eneo la Jiweni Kabamba katika tarafa ya
Kibosho wilayani Moshi.
Mutafungwa alisema, mtalii huyo aliingia nchini Septemba 3, kupitia
Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), uliopo wilayani Hai.
Alisema madhumuni ya kuingia nchini ni kupanda mlima huo ambao ni mrefu
zaidi barani Afrika.
Alisema raia huyo alikuwa na hati ya kusafiria yenye namba E 43941406 na
kwamba uchunguzi wa awali ulionesha kuwa kifo chake kilisababishwa na
magonjwa yanayotokana na kubadilika kwa hali ya hewa.
Alisema mwili wa marehemu umehifadhiwa kwenye Hospitali ya Rufaa ya KCMC
katika Manispaa ya Moshi, kwa ajili ya uchunguzi zaidi, huku taratibu
za kuusafirisha mwili zikiendelea. Mwaka huu watalii wawili wamepoteza
maisha kwenye ajali wakati wakifanya utalii.
Kifo cha kwanza kiliripotiwa kutokea mwaka huu, baada ya raia wa Afrika
Kusini, Gululeth Zulu (38) kushindwa kupumua akiwa kwenye mwinuko wa juu
ya mlima. Kifo hicho kilitokea Julai 18.
No comments:
Post a Comment