Mfanyabiasha Leonard Materu (31) amepandishwa kizimbani katika Mahakama
ya Hakimu Mkazi Kisutu, akikabiliwa na mashitaka ya kutuma ujumbe wa
kumtishia Rais John Magufuli kupitia mtandao wa WhatsApp.
Materu ambaye ni mkazi wa Moshi Bar Kwadiwani, alifikishwa mahakamani
hapo jana na kusomewa mashitaka yake na Wakili wa Serikali, Diana
Lukondo mbele ya Hakimu Mkazi Magreth Bankika.
Akisoma mashitaka Wakili Diana alidai, mshitakiwa huyo amefunguliwa kesi
hiyo ya kuchapisha taarifa za uongo kwenye mtandao wa WhatsApp chini ya
Sheria ya Mtandao ya mwaka 2015.
Ilidaiwa kuwa, Julai 17, mwaka huu jijini Dar es Salaam, Materu
aliandika ujumbe wenye lengo la kudanganya umma kupitia WhatsApp
ukisomeka; “Magu ajiandae tunaenda kupindua mpaka Ikulu.”
Inadaiwa kuwa maneno hayo yalikuwa na lengo la kumtishia Rais John
Magufuli. Baada ya kusomewa mashitaka, mshitakiwa alikana kutenda kosa
hilo, na upande wa Jamhuri ulidai kuwa upelelezi wa kesi haujakamilika
na kuomba tarehe nyingine ya kutajwa.
Mshitakiwa aliachiwa kwa dhamana baada ya kutimiza masharti ya dhamana
ya kuwa na wadhamini wawili ambao kila mmoja alisaini hati ya Sh milioni
tano. Kesi itatajwa tena Septemba 20, mwaka huu.
No comments:
Post a Comment