Friday, 9 September 2016

WARAKA KWA MWALIMU RAZAQ MTELE MALILO, KATIBU WA CUF, TAWI LA CHUO KIKUU CHA DAR ES SALAAM.

WARAKA KWA MWALIMU RAZAQ MTELE MALILO, KATIBU WA CUF, TAWI LA CHUO KIKUU CHA DAR ES SALAAM.
Ndugu Mwl Razaq Mtele Malilo, nimelazimika kuishika kalamu yangu na kukuandikia waraka huu baada ya wewe kufanya kitendo cha kiungwana cha kuandika mabandiko ya mtandaoni kunipongeza mara mbili. Mara ya kwanza ilikuwa wakati nilipoteuliwa kushika nafasi ya Ukatibu wa Itikadi na Uenezi kwenye chama cha ACT Wazalendo. Mara ya pili ni hapa majuzi wakati mgogoro wa CUF ulipoanza kuchipua.
Kwenye maandiko yako yote mawili, umeeleza hisia zako chanya juu yangu. Mathalani, kwenye andiko lako la awali, ulieleza waziwazi imani yako kuwa mimi “ni kijana makini” na kunisihi kuwa “Chama kisinifanye kuacha misimamo yangu na kuwa kama TV inayoendeshwa kwa Rimoti”. Majuzi ukarudia tena kuwa “licha ya utofauti wa kiitikadi, mimi ni moja ya viongozi wanaochipukia unaowaheshimu sana na kwamba unajifunza mengi kutoka kwangu. Sina hakika kama ninastahili sifa zote hizi lakini sina budi kukushukuru na kuziheshimu hisia zako, hisia kutoka kwenye kinywa cha kijana mwanaharakati!
Kwa sifa hizo pomoni ulizonimiminia, nitastahili jina gani nami nisipokuandikia zaidi ya jina la “Mtu mwenye kujivuna asiyethamini pongezi?”
Kwa bahati mbaya ninalazimika kukuandikia juu ya jambo ambalo nilichukua msimamo wa kutolizungumzia sana kwa sababu ya kuziheshimu hisia zangu juu ya jambo lenyewe. Lakini, kwa sababu watu mbalimbali, wewe ukiwemo, wamekuwa wakinitaja kwa wema kabisa kwenye mijadala mikali juu ya suala la CUF, ni bora nami nitoe mchango wangu kiasi.
Ingwa sijawahi kuwa mwanachama wa CUF, sioni soni kusema kwamba mimi nimezaliwa, kukulia na kusoma (Shule ya msingi hadi kidato cha sita) kwenye maeneo ambayo CUF ilikuwa na ushawishi mkubwa. Kumbukumbu zangu zinanirudisha nyuma miaka mingi wakati wa uchaguzi wa mwaka 2000. Kwetu, siku za mwisho wa wiki, hasa kipindi cha baridi tulikuwa na desturi ya kuota moto pamoja asubuhi ambao tuliuita “Liburiburi”. Kwangu, ilikuwa ni desturi kujumuika kwenye Liburiburi na Mzee Adam (Radhi za Mola ziwe juu yake) aliyeishi jirani yetu na watu wengine. Wakati huo, japo sikufikisha umri wa kupiga kura, nilivutiwa sana na simulizi za kwenye Liburiburi ambazo zilitolewa kuhusu Chama cha CUF na mgombea wake Prof. Ibrahim Haruna Lipumba. Nilihamasika sana na sifa za usomi wa Prof. Lipumba zilizomwagwa na Mzee Ngulungu aliyekuwa bingwa wa kutawala mazungumzo kwenye Liburiburi (Ingawa baadaye nilifahamu kuwa zilitiwa chumvi sana hasa imani tuliyopewa kwenye Liburiburi kuwa yeye ni Mchumi bora Namba moja dunia nzima!).
Pia, kampeni zilipopamba moto mimi na vijana wenzangu tulikwenda mara nyingi nyumbani kwa Mzee Abdallah Khalifa, moja ya waliokuwa Maalwatan wakubwa kabisa wa CUF Tunduru kutazama video za hotuba na ziara za Prof. Lipumba na viongozi wengine wa CUF. Wakati huo, video ilikuwa 'issue' kwelikweli! Kwa kweli ile nyimbo “Ohhh Ohh Chama, Chama gani? Chama cha Wananchi CUFFFFFFFFF ilinikaa sana kipindi hicho”
Kila viongozi wa CUF walipokutana na mkono wa propaganda za dola mimi nilihuzunika sana. Tukio ninalolikumbuka zaidi ni la Polisi waliomvamia Alhaj Omari Kweja Mfaume, Mgombea ubunge wa CUF Tunduru na kuisachi nyumba yake kwa mikwara wakimfungamanisha na ujangili. Sote tunajua hiyo ilikuwa ni ghirba ya CCM kumdhoofisha.
Tajirba (Experience) hii ilinifanya, mwaka 2005, nikiwa Ndanda Sekondari kuipigia kura CUF kuanzia udiwani, ubunge hadi urais. Hata mwaka 2011, miezi michache kabla sijafukuzwa chuo kikuu cha Dar es salaam kutokana na vuguvugu la kukosoa mfumo mbovu wa ugawanyaji wa mikopo ya wanafunzi wa vyuo vikuu, nilimwandikia Ndugu Julius Mtatiro juu ya umuhimu wa CUF kuwekeza vyuo vikuu. Naye bila ya hiyana, alinielekeza kwenda Makao Makuu ya CUF Buguruni na kunikutanisha na Ndugu Thomas Malima aliyekuwa Naibu Katibu wa Jumuiya ya Vijana ya CUF (JUVICUF). Ingawa hadi muda huo sikuwa na nia ya kujiunga na chama chochote cha siasa, nili-syphasize sana na CUF kutokana na makuzi yangu.
Nilipokata shauri kujiunga na siasa za vyama sikwenda CUF kwa sababu ya itikadi tuu. Nyinyi awali mlikuwa wana “Utajirisho” na baadaye “Waliberali” wakati mimi, hasa baada ya malezi ya kiuanazuoni nikiwa UDSM, ninaushika mkono ujamaa. Lakini, hili halijawahi kuondoa udugu wangu na CUF na baadhi ya viongozi na wanachama wake, waandamizi kwa chipukizi, wewe ukiwemo.
Hivi majuzi, baada ya mzozo wa CUF kufukuta na baadaye kuleta sintofahamu kubwa, mimi nilifuatilia nukta kwa nukta. Na kwa ajabu (Japo ilitufaa wengi) Chama kiliamua kurusha Live sehemu kubwa ya mkutano ule wenye ajenda tete!
Kwa kweli, ni lazima tukiri CUF mpo kwenye mtihani mkubwa! Binafsi, nilipokata shauri kukaa kimya, niliamini kuwa pengine baada ya mtifuano, “Wakubwa” ndani ya Chama watakumbuka maslahi ya Chama ni bora kuliko maslahi yao binafsi na kutafuta muafaka. Kwa kweli, laiti viongozi wangekumbuka damu za watu, mikasa ya watu, utu wa watu uliovunjwa bila sababu kwa sababu ya CUF, basi wengi wangekubali “kufa kidogo” ili CUF ipone. Lakini kwa hali ilipofikia, ni dhahiri hakuna aliye tayari kuachia kamba!
Binafsi nina amini kuwa mgogoro wa CUF unalizoofisha sana vuguvugu la upinzani nchini. Ndiyo maana nilimwandikia rafiki yangu Amar Ali (Mwana CUF anayeishi ughaibuni) kuwa mnufaika namba moja wa mgogoro wa CUF ni Chama cha Mapinduzi, hasa Dk. Shein ambaye sasa atavuta pumzi kidogo kwa sababu Maalim Seif anashughulishwa sana na mgogoro wa ndani.
Lakini, mbali na CCM, vipo vyama vingine vyenye maslahi kwenye mzozo huu hasa ACT na CHADEMA. Wewe unajua mengi na sina haja ya kukufahamisha. ACT, chama ambacho mimi ni mwenezi wake, kwa vyovyote vile, kama wana CUF hawatapatana, kitakuwa ni moja ya kimbilio la wataoshindwa kuendelea CUF. Hata nyinyi wenyewe mmeshawapa nembo ya ACT wanaomuunga mkono Prof. Lipumba na wewe umeshawahi kuandika kuwataka waende mapema “vidole vitano” ili “Wawapishe mpumue”. Yupo kiongozi mwandamizi wa CUF Tunduru, yeye hunipigia simu kirafiki kabisa na kunihimiza “Ado hata kama hawajawafuata, wafuateni nyie muwachukue ili sisi tupumue!”. Hili linakolezwa pia na mahusiano ya kirafiki, kitaaluma na kisiasa tangu huko nyuma kati ya Prof. Lipumba na Ndugu Zitto Kabwe, Kiongozi wa Chama wa Act Wazalendo. Haishangazi hivyo basi magazeti yakiandika kila leo kuwa Lipumba na wafuasi wao watatimkia ACT. Lakini, kwani Ndugu Malilo hili ni jipya? Hata Ndugu Lwakatare na Abdallah Safari ambao sasa ni "vingunge" CHADEMA si walikuwa CUF? Kwa hiyo, ikitokea mtu akavutiwa kuja kwetu, ilimradi akubali misingi yetu, unadhani tutamkataa?
CHADEMA nao wana maslahi yao kwenye linaloendelea CUF. Kama ambavyo viongozi wa ACT wanasemwa kulizungumzia suala la CUF, viongozi waandamizi wa CHADEMA nao wanasema kila leo juu ya sakata lenu. Hata katika kikao (Na kwa bahati kumbukumbu za video zipo) baadhi ya wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CUF walikituhumu CHADEMA kuingilia suala la CUF ikiwemo kutoa ulinzi kwa mkutano. Mimi sina ushahidi nalo. Unafahamu kwa nini CHADEMA wana maslahi kwenu? Jibu ni jepesi: Wana hofu kama Lipumba au hata wafuasi wake watashika hatamu CUF, UKAWA utakuwa mashakani.
Yote kwa yote ni kwa maslahi ya vuguvugu la upinzani nchini mvuke salama na CUF kama chama kibaki. Nami, nikikumbuka zama zangu za kwenye Liburiburi, ninawaombea kila la heri ingawa ni vigumu sana, kwa maoni yangu, upande mmoja kutoondoka ili, kama usemavyo “CUF ipumue”.
Wasalimie sana Lindi ambako najua upo likizo.
Nduguyo,
Komredi Ado Shaibu
Mwana wa kijiji cha Namasakata,
Wilaya ya Tunduru.

No comments:

Post a Comment