WASICHANA wengi hasa walio na uwezo wa kushika mimba ambao wanasoma au
hawajaolewa wamekuwa wakijihusisha na matukio ya kutoa mimba mara kwa
mara bila kufikiria athari za kutoa mimba kwa uzito.
Athari hizo ni pamoja na kuweka maisha hatarini, kuharibu kizazi,
kujiweka katika hatari zaidi ya kupata maradhi kama Saratani ya Shingo
ya Kizazi, kushitakiwa na nchi kwa kosa la kuua pamoja na kuharibu
uhusiano wao na Mungu.Machaguo ya Kuzuia Mimba kwa Vijana walio
Masomoni :-
Kusubiri wakati unaofaa
Vijana wanatiwa moyo kusubiri na dini zao na walezi wao, ingawa hata
serikali ina sheria zinazopendekeza umri sahihi kujihusisha na ngono.
Kijana anaweza kuamua kibinafsi kusubiri muda muafaka na kuwa na mtu
sahihi.
Kusubiri kutakuweka salama na bila wasiwasi wowote wa kuambukizwa
magonjwa yanayoenezwa kwa njia ya ngono. Kuwa salama kutakufanya kukazia
malengo yako ya maisha.
Maamuzi ya kusubiri wakati unaofaa hakutakufanya mihemko ya ngono
kupotea bali itakubidi kukazia fikra mambo ya msingi katika maisha yako
badala ya kuwaza ngono.
Ngono salama
Waopendwa wasomaji wa Gazeti hili mtandao la FikraPevu hapa
ninamaana ya kutumia njia ambazo zinazopunguza uwezekano wa kupata
mimba au magonjwa ya ngono ukitia ndani Virusi vya UKIMWI (VVU). Mihemko
ikikuzidi na ukashindwa kusubiri wakati unaofaa kuanza ngono ni bora
kujilinda wewe na mwenzi wako kwa kutumia kinga.
Mipira (Kondom) ndio njia pekee itakayokukinga usipatwe na ujauzito na
magonjwa ya ngono ikiwemo VVU, wakati huo huo hutumika kama njia ya
uzazi wa mpango.
Vidonge vya dharura vya Uzazi wa Mpango
Ikitokea umefanya ngono bila kinga ya kondom hasa kwa mtoto wa kike
ambaye hakuwa anatumia njia za uzazi wa mpango inashauriwa kutumia
vidonge vya dhalula vya uzazi wa mpango ili kuzuia mimba isiyotarajiwa
ingawa vidonge hivyo havitasaidia kupunguza hatari ya kuambukizwa na
magonjwa ya ngono ikiwemo VVU.
Vidonge vya dharura vya uzazi wa mpango ni vidonge vya vya uzazi wa
mpango ambavyo ni vya aina kuu mbili, vidonge vyenye vichocheo viwili
vitwavyo Estrojeni na Projesteroni na vidonge vyenye kichocheo kimoja tu
cha Projesteroni.
Vidonge vya dharura vya uzazi wa mpango vipo vya aina tofauti na zina
nguvu tofauti, kuna zinazopaswa kutumika ndani ya masaa 72 (Siku 3)
baada ya ngono isiyo salama na kuna zinazopaswa kutumika ndani ya masaa
120 (Siku 5) baada ya ngono isiyo salama.
Aina zote za vidonge vya dharura vya uzazi wa mpango hufanya kazi ya
kuzuia mimba kwa kuzuia Ouvuleshaji ambapo huzuia au kuchelewesha yai
kutoka kwenye kokwa (Foliko za Graaf) zilizomo katika Ovari.
Katika hali zisizotarajiwa, mabinti hubakwa na watu wasiowafahamu hali
zao za afya. Ikiwa umetokewa na hali hiyo tafuta ushauri wa kitiba
haraka sana. Katika hali hiyo unaweza kumeza vidonge vya dhalula ndani
ya saa 72 hadi 120 tangu ulipofanya ngono ili kuzuia mimba. Pia daktari
anaweza kukupima VVU na kukupa vidonge vitakavyo kukinga na VVU ikiwa
haijulikani hali ya VVU ya mbakaji.
Vidonge vya dhalula vya uzazi wa mpango vinaweza kutumika kabla ya
ngono isiyo salama kama una hofu na njia ya uzazi wa mpango unayotumia
sasa, kama unaenda likizo na hutoweza kupata vidonge vya dhalula vya
uzazi wa mpango. Muulize daktari au muuguzi ili upate taarifa kamili
kuhusu kutumia vidonge vya dhalula vya uzazi wa mpango kabla ya ngono
isiyo salama.
Baada ya kutumia vidonge vya dhalula vya uzazi wa mpango ikiwa hedhi
yako itachelewa zaidi ya siku 7 au ni nyepesi au ya muda mfupi sana
wasiliana na mtaalamu wa afya ili kupima mimba kwanza.
Athari zinazojitokeza mara kwa mara baada ya kutumia vidonge vya
dhalula vya uzazi wa mpango ni pamoja na maumivu ya tumbo, kuumwa
kichwa, hedhi kubadilika badilika inaweza kuwa matone tu au nyingi
zaidi, kujihisi uchovu na kuumwa.
Athari zinazojitokeza kwa uchache ni pamoja na matiti kujaa na kuuma,
kizunguzungu na kutapika. Ni busara kuwasiliana na mhudumu wa afya ya
uzazi ikiwa utapatwa na dalili zisizo za kawaida.
Vidonge vya dhalula vya uzazi wa mpango vinaathiriwa na dawa zingine
kama za kutibu Kifafa, VVU, Kifua Kikuu na Vidonda vya Tumbo. Hivyo
wasiliana na mtaalamu wa huduma za uzazi wa mpango kabla ya hujatumia
vidonge vya dharura vya uzazi wa mpango.
Kitanzi (Intrauterine Device)
Kitanzi kinaweza kuwekwa kwenye uterasi ogani ambamo utungo wa mimba
hupokolewa na kustawishwa ndani ya masaa 120 (Siku 5) baada ya ngono
isiyo salama au siku 5 kabla ya Ouvuleshaji. Kitanzi kinaweza zuia yai
kurutubishwa na mbegu ya kiume. Wanawake chini ya asilimia 1 wanaotumia
kitanzi ndio wanaweza kupata mimba.
Kitanzi ni kifaa kidogo chenye umbo la T kilichotengenezwa kwa plastiki na kopa (Copper).
Kifaa hiki huingizwa kwenye uterasi/kizazi (ogani ambamo utungo wa
mimba hupokelewa na kustawishwa) na mtaalamu wa afya mwenye utaalamu
huo. Kifaa hiki kinafanya kazi kwa kuzuia yai kurutubishwa na mbegu ya
kiume (manii).
Kuna aina nyingi za Vitanzi. Aina mpya zina kopa zaidi na zina ufanisi
zaidi ya asilimia 99. Wanawake chini ya wawili kati ya wanawake 100
wanaotumia aina mpya kwa zaidi ya miaka 5 ndio wanaoweza kupata mimba.
Vitanzi vyenye kopa kidogo vina nguvu kidogo ukilinganisha na vyenye
kopa nyingi ila bado vinaweza kuzuia mimba.
Ikiwa umefanya ngono isiyo salama, kitanzi kinaweza kuwekwa ndani ya
siku 5 baada ya ngono isiyo salama na kuweza kuzuia mimba. Ni njia
madhubuti ya kuzuia mimba kuliko vidonge vya dharura vya uzazi wa mpango
na pia hakiingiliani na dawa zingine. Unaweza pia kuamua kukiacha kama
njia yako ya uzazi wa mpango.
Mara nyingi wanawake wengi wanaweza kutumia kitanzi kwa kukiingiza
ndani ya uke na wale ambao hawakuwahi kushika mimba, wanaonyonyesha na
wale wenye VVU. Mtaalamu wa afya ya uzazi atakuuliza juu ya historia
yako ya matibabu ili kufahamu kama kitanzi kitakufaa.
Hupaswi kutumia kitanzi kama una ugonjwa wa zinaa au maambukizi kwenye
via vya uzazi, ukiwa na kasoro ya maumbile kwenye mlango wa uzazi au
unatokwa na damu ukeni hasa baada ya tendo la ndoa au baada ya hedhi.
Wanawake waliopata mimba nje ya fuko la kizazi au walio haribu mimba
hivi karibuni au wanaotumia vifaa bandia vya moyo wanapaswa kuwasiliana
na daktari kabla ya kuwekewa kitanzi.
Athari za kutumia kitanzi ni chache ila mtu anaweza kupata maumivu,
maambukizi ya njia ya mkojo na kizazi. Kama utatumia kitanzi kama njia
yako ya uzazi wa mpango, kitafanya siku zako za hedhi kuwa nyingi zaidi
pamoja na kutokwa na hedhi nyingi na maumivu zaidi. Kama unahisi vibaya
au maumivu baada ya kuweka kitanzi, kutumia dawa za kutuliza maumivu
zinaweza kutumika kupunguza tatizo.
No comments:
Post a Comment